Local Bulletins

Wasomi Warendile waunga mkono BBI, wataka 12% ya mgao wa kaunti kutengwa kwa ajili ya ufugaji

A Rendile homestead in Marsabit. Photo courtesy of office of the Governor Marsabit

By Adano Sharamo

Jamii ya Rendille kupitia muungano wa Wasomi wa jamii hiyo Rendille Professionals’  Association RPA wametangaza kuunga mkono Ripoti ya Upatanisho BBI. 

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Sunya Owre viongozi wa RPA wametoa mapendekezo yao 9 wanayodhamiria kuwasilisha wakati wa mkutano wa BBI unaotarajiwa kuandaliwa mjini Isiolo.

Kati ya mapendekezo yao ni kuundwa kwa nafasi ya kiongozi wa upinzani atakayefanya kazi kwa karibu na bunge la kaunti, kuongezwa kwa mgao wa serikali ya kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35, kuundwa kwa fedha za ustawi wa wadi kando na kuongezwa kwa fedha za ustawi wa maeneo bunge kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 5.

Mapendekezo mengine ni kutengwa kwa asilimia 12 ya fedha za kaunti kwa minajili ya kuimarisha sekta ya ufugaji na kulindwa kwa ardhi za jamii kupitia kuidhinishwa kwa sheria za ardhi chini ya katiba.

Wasomi hao wamesema aidha, wanapinga pendekezo la kuundwa kwa serikali za kimaeneo na wanapendekeza pia kuundwa nafasi maalum za uongozi kwa ajili ya jamii ndogo humu jimboni.

Wasomi wamesema wako tayari kusikiliza mapendekezo yatakayotolewa na jamii zingine kwa ajili ya kuwaunganisha wakazi wa kaunti hii.
Wametoa wito kwa viongozi kutopinga mapendekezo ya BBI badala yake kusaidia katika kurekebisha vipengele ambavyo vitaonekana kuwa na utata.

Subscribe to eNewsletter