Zaidi ya watu 134,000 wahitaji msaada wa dharura wa chakula Marsabit
Na JB Nateleng
Licha ya Kaunti ya Marsabit kupokea mvua mwishoni mwa mwezi wa pili hadi mwanzoni mwa mwezi wa tatu, maelfu ya wakaazi bado wanakabiliwa na uhaba wa chakula na wanahitaji msaada wa dharura.
Kwa mujibu wa Afisa wa Mawasiliano katika Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabili Ukame na Majanga (NDMA) tawi la Marsabit, John Ougo, takriban watu 134,750 wanahitaji msaada wa chakula kwa haraka akisema kuwa hali hii imesababishwa na wafugaji kupoteza mifugo pamoja na wakulima kushindwa kupata mavuno ya kutosha mwaka uliopita.
Ougo amesema kuwa hali hiyo ya uhaba wa chakula imechangia ongezeka la visa vya utapiamlo jimboni.
Maeneo ya North Horr na Laisamis yapo juu ya asilimia 15 ya kiwango cha utapiamlo, huku Moyale na Saku zikiripotiwa pia kuwa katika hali mbaya zaidi ya utapiamlo.
Aidha, afisa huyu ameeleza kuwa hali hii huenda ikaendelea kuzorota kutokana na athari za kiangazi pamoja na mvua kubwa inayoweza kushuhudiwa katika Kaunti ya Marsabit.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kaunti ya Marsabi ilipokea mvua inayozidi wastani mwanzoni mwa mwezi wa tatu, huku akiwatahadharisha wakazi kuwa waangalifu zaidi msimu huu wa mvua unaotarajiwa mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi wa nne.



Post Comment