Highlights

Usalama waimarishwa Marsabit Central kuelekea sherehe ya Idd-Ul-Fitr kesho Ijumaa

Na Caroline Waforo

Idara ya usalama katika kaunti ndogo ya Marsabit Central imewahakikishia wakaazi usalama wa kutosha wakati ya sherehe ya Idd-Ul-Fitr siku ya hapo kesho Ijumaa.

Akizungumza na Shajara OCPD wa Marsabit Central Beethoven Gachago, amesema kuwa maafisa wa polisi wameimarisha doria ili kuhakikisha kuwa waumini wa dini ya Kiislamu wanasherehekea kwa utulivu.

Aidha amewahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema kuhusu mienendo yoyote ya kutiliwa shaka ili kuzuia visa vya uhalifu.

Hapo jana Jumatano Wizara ya Usalama wa Taifa ilitangaza kesho Ijumaa, Machi 20, kuwa sikukuu ya Idd-Ul-Fitr.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen alichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa kesho itakuwa sikukuu.

Sikukuu ya Idd husherehekewa na Waislamu wote kote duniani kuashiria kukamilika kwa siku 30 za mfungo wa Ramadhani.

Mfungo wa Ramadhani huwa ni mwezi mtakatifu kwa Waislamu ambao hufunga kula na kunywa kutoka macheo hadi machweo wakipiga dua.

Ramadhani ni mojawapo wa nguzo kuu tano za dini ya Uislamu, na sherehe za Idd huadhimisha kukamilika kwa mfungo huku ndugu, jamaa na marifiki wakiandaa sherehe na pia kuwakumbuka wasiobahatika katika jamii wakati wa Idd kwa kula pamoja au kutoa msaada wa vyakula.

Post Comment