Wafugaji na wakulima waombwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Marsabit
Na Sabalua Moses
Wafugaji na wakulima katika kaunti ya Marsabit wametakiwa kukumbatia mabadiliko ya tabia nchi ili kuimarisha mikakati ya kupunguza athari zake na kulinda mazingira.
Kulingana na Naibu Gavana wa Kaunti ya Marsabit, Solomon Gubo, ni muhimu kwa washkadau mbalimbali kuwaelimisha wakulima na wafugaji kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza katika mkutano uliowaleta pamoja wadau mbalimbali kwa lengo la kuangazia mabadiliko ya tabianchi Gubo amesema elimu hii itawawezesha kufanya maamuzi sahihi katika kilimo na ufugaji, na hivyo kuwahakikisha usalama wa chakula.
Vile vile naibu gavana amewahimiza wafugaji kulinda misitu na vyanzo vya maji kwa manufaa ya vizazi vijazo.
Pia amesisitiza umuhimu wa kupunguza idadi ya mifugo, hasa katika kipindi cha mabadiliko ya tabia nchi, ili kuepuka uharibifu wa mazingira na uhaba wa malisho.
Mkutano huo uliwaleta pamoja washikadau kutoka idara za mifugo, kilimo, utabiri wa hali ya hewa, mamlaka ya kudhibiti ukame (NDMA), pamoja na viongozi wa serikali, kwa lengo la kujadili mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.



Post Comment