Watu sita wauawa huku wanane wakijeruhiwa katika shambulizi la wizi wa mifugo illeret, mpakani mwa kenya na ethiopia
Na Mwandishi Wetu
Watu sita wameuawa huku wengine wanane wakijeruhiwa vibaya katika shambulizi la wizi wa mifugo katika eneo la Illeret kaunti ya Marsabit mpakani mwa Kenya na Ethiopia.
Akithibitisha shambulizi hilo Mratibu wa Ukanda wa Mashariki Paul Rotich amesema kuwa majangili kutoka taifa jirani la Ethiopia walitekeleza uvamizi huo jana Jumanne na kutoweka na mbuzi 1,400 pamoja na ngombe 500.
Rotich amesema kwamba majeruhi wanapokea matibabu katika hospitali mbalimbali ikiwemo vituo vya matibau katika eneo hilo la Illeret.
Aidha vikosi vya usalama vinashika doria katika eneo hilo ili kurejesha hali ya utulivu na kuzuia mashambulizi ya kulipiza kisasi. Vile vile juhudi za kufuatilia na kurejesha mifugo iliyoibwa zinaendelea.
Ripoti zinaashiria kuwa mazungumzo ya pande zote mbili yameanza ili kutuliza joto.
Itakumbukwa kuwa kaunti ya Marsabit ni miongoni mwa kaunti zilizokuwa chini ya operesheni Maliza Uhalifu, operesheni iliyolenga kukabiliana na ujangili na uhalifu wa wizi wa mifugo.
Kaunti nyingine ni pamoja na Isiolo, Meru, Turkana, West Pokot pamoja na Baringo.



Post Comment