Wanawake Marsabit watakiwa kujitokeza kufanyiwa vipimo vya saratani ya mlango wa kizazi.
NA JB Nateleng
Huku dunia ikitenga mwezi huu wa kansa kuwa mwezi wa kutoa hamasa kuhusu saratani ya nyumba ya Uzazi (Cervical Cancer), Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Marsabit kuweza kuacha tamaduni zinazosababisha kuenea kwa saratani ya nyumba ya uzazi.
Ndoa za mapema imetajwa kama mojawapo ya tamaduni ambayo inasababishia msichana kupata saratani ya nyumba ya uzazi huku hamasa ikizidi kutolea zaidi kuhusu mila hii potovu.
Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya kipekee daktari anayeshughulia magonjwa ya wanawake katika hospitali ya rufaa ya Marsabit Daki Halake amesema kwamba ni sharti Watoto wa kike walindwe dhidi ya hii mila potovu ili kuwakinga na ugonjwa huu wa saratani ambayo ameitaja kama jinamizi inayoangamiza mtu polepole.
Daki ametaja pia kuwa na wapenzi wengi kunachangia kuenea kwa saratani hii huku akitoa wito kwa wachumba kuwa waaminifu katika ndoa yao.
Kutokwa na damu kwenye sehemu ya siri kila mara na kuhisi uchungu wakati wa tendo la ngono imetajwa kama dalili ya saratani ya nyumba ya uzazi.
Kadhalika Daki amewarai wasichana pamoja na wanawake kutembelea zahanati iliyopo karibu nao ili kupata chanjo ya HPV ambayo itawasaidia kujikinga na ugonjwa huu.



Post Comment