Wakazi wa Saku walalamikia uhaba wa maji
Na JB Nateleng
Wakazi wa eneo bunge la Saku kaunti ya Marsabit wameitaka kampuni ya kusambaza maji ya Marsabit (MARWASCO) kuingilia kati haraka ili kurejesha huduma ya maji katika maeneo yao.
Wakizungumza na Shajara, wakazi hao wamesema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji muda mfupi baada ya mvua kukoma, hali ambayo imewalazimu kutegemea wachuuzi wa kibinafsi wanaouza maji kwa bei ya juu.
Wakazi hao wanasema gharama ya maji imeendelea kupanda na sasa inaathiri shughuli zao za kila siku za nyumbani pamoja na maisha yao kwa ujumla.
Kilio hicho kinajiri saa chache baada ya kuibuka madai kuwa kampuni ya kusambaza umeme nchini, Kenya Power, tawi la Marsabit, imeikatia umeme kampuni ya MARWASCO kutokana na deni.
Uchunguzi wa kituo hiki umebaini kuwa ni kweli Kenya Power ilikata umeme wa kampuni hiyo kwa sababu ya deni, ingawa haijaweka wazi kiwango kinachodaiwa.
Hata hivyo, juhudi za kituo hiki kupata maoni kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa MARWASCO, Stephen Katelo, hazikufanikiwa kufikia wakati taarifa hii ikienda hewani kwani alikuwa katika mkutano.



Post Comment