Matumizi ya bidhaa za tumbaku yaongezeka miongoni mwa wanafunzi Marsabit
Na JB Nateleng
Matumizi ya bidhaa za tumbaku miongoni mwa wanafunzi katika Kaunti ya Marsabit yameripotiwa kuongezeka, kwa mujibu wa Mratibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya na Mihadarati (NACADA) tawi la Marsabit, Mohammed Wako.
Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya simu, Wako amesema watoto wengi huanza kutumia mihadarati wakiwa na umri mdogo, hali inayochangia kudorora kwa masomo yao na kuathiri maendeleo yao ya kielimu.
Ameeleza kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ndio wanaoathirika zaidi, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha kampeni za uhamasishaji kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku mashuleni.
Wako pia ameonya kuhusu kuibuka kwa aina mpya za bidhaa za tumbaku zisizo na harufu, akisema kuwa hali hiyo inaongeza uwezekano wa vijana na wanawake kuzitumia bila kutambuliwa kwa urahisi.
Aidha, amebainisha kuwa malezi ya nyumbani yanachangia pakubwa kuenea kwa tabia hiyo, akieleza kuwa watoto mara nyingi huiga mienendo ya wazazi wao na marafiki wanaowazunguka.
Mohammed ameitaka jamii kuwa makini katika kukabiliana na matumizi ya tumbaku, akionya kuwa bidhaa hizo zinaweza kusababisha magonjwa hatari kama saratani ya mapafu pamoja na magonjwa mengine yanayoathiri figo na ubongo.



Post Comment