Highlights

Wakazi wa Marsabit Wahimizwa kutembelea vituo vya afya ili kupimwa kifua kikuu (TB)

Na JB Nateleng

Wakazi wa Marsabit wamehimizwa kutembelea vituo vya afya vilivyo karibu nao mara wanapoanza kuonyesha dalili za ugonjwa wa kifua kikuu (TB), hasa kikohozi cha muda mrefu, ili kupimwa na kuanza matibabu mapema.

Wito huo umetolewa na Msimamizi Mkuu wa masuala ya kifua kikuu katika kaunti ya Marsabit Sori Gone, ambaye amesema ugonjwa wa TB bado upo na unahitaji umakini wa jamii akisisitiza kuwa mtu yeyote anayehisi dalili zisizo za kawaida mwilini anapaswa kufika hospitalini haraka.

Akizungumza na idhaa hii akiwa ofisini mwake, Sori amesema ugonjwa huo unaweza pia kuambukizwa kwa watoto, hasa pale mzazi au mlezi aliyeathirika anapokuwa karibu nao bila tahadhari.

Wakati huo huo, Sori amesema kumekuwa na kupungua kwa visa vya wagonjwa wanaokatiza matibabu ya TB kabla ya kukamilika.

Hata hivyo, ameeleza kuwa baadhi ya changamoto bado zipo, hususan miongoni mwa watu wanaotumia pombe kupita kiasi na mihadarati, ambao mara nyingi hushindwa kufuata masharti ya matibabu.

Post Comment