Papa Leo XIV akubali Kujiuzulu kwa Askofu Paul Kariuki Njiru wa Jimbo la Wote
Na JB Nateleng
Papa Leo XIV amekubali rasmi kujiuzulu kwa Askofu Paul Kariuki Njiru, aliyekuwa askofu mwanzilishi wa Jimbo Katoliki la Wote.
Katika hatua hiyo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Mhashamu Askofu Simon Peter Kamomoe, kuwa msimamizi wa kitume, akisimamia uongozi wa kichungaji na kiutawala wa jimbo hilo katika kipindi cha mpito.
Tangazo hilo lilitolewa mjini Roma tarehe 25 Machi 2026 saa sita mchana kwa majira ya Vatican, sawa na saa nane mchana kwa saa za Kenya, na kuwasilishwa rasmi kwa Maaskofu wa Kenya kupitia Balozi wa Kitume nchini Kenya, Askofu Mkuu Bert Van Megen.
Askofu Paul Kariuki Njiru alizaliwa tarehe 11 Machi 1963 huko Kathunguri, Kaunti ya Embu. Alipata mafunzo ya falsafa katika Seminari ya Mtakatifu Joseph, Meru, na theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Thomas Aquinas, Nairobi, kabla ya kutawazwa kuwa kasisi tarehe 1 Machi 1993.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Wote, Askofu Kariuki amewahi kuhudumu kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Embu kuanzia mwaka 2009 hadi 2023, kufuatia uteuzi wake na Papa Benedict XVI.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kujiuzulu kwake kunahusishwa na changamoto za kiafya alizokuwa akikabiliana nazo katika siku za hivi karibuni, hali iliyosababisha pia uteuzi wa askofu msaidizi katika jimbo hilo.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya utaratibu wa kichungaji unaolenga kuimarisha uongozi na huduma kwa waumini wa jimbo katoliki la Wote



Post Comment