Highlights

IPOA kufungua afisi zake Marsabit huku visa 121 vya dhulma za polisiĀ  vikiripotiwa hadi kufikia sasa

Na Caroline Waforo

Jumla ya visa 121 vya ukiukaji wa haki za binadamu vinavyohusisha maafisa wa polisi katika kaunti ya Marsabit vimeripotiwa kwa Tume ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi IPOA.

Haya yamebainika wakati wa kikao cha kuhamasisha umma kuhusu majukumu na utendakazi wa tume hiyo, kilichofanyika leo Ijumaa katika ukumbi wa Kanisa Katoliki.

Akizungumza na wanahabari Afisa Mkuu Mtendaji wa IPOA Elema Halakhe amedokeza kuwa kesi hizo zilizoripotiwa tangu kwasisiwa kwa IPOA, zinajumuisha madai ya utekaji nyara, ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka kati ya kesi nyinginezo.

Ameongeza kuwa baadhi ya kesi hizo tayari zimefikishwa mahakamani huku nyingine zikiendelea kuchunguzwa zikiwemo zinazotoka maeneo ya Sololo na Moyale.

Aidha amedokeza kuwa idadi kubwa ya kesi zilizoripotiwa wakati wa operesheni Ondoa Jangili Marsabit tayari zimesuluhishwa.

Wakati huo huo IPOA inafungua afisi zake hapa katika kaunti ya Marsabit, hatua ambayo kamishna wa tume hiyo Muchiri Nyagah amesema inalenga kuleta huduma karibu za mwananchi.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao hicho wamepongeza hatua hiyo wakisema kuwa itasaidia kushughulikia malalamishi dhidi ya maafisa wa polisi hasa katika juhudi za kupambana na ulanguzi wa mihadarati na dawa za kulevya ambapo maafisa wa polisi wamedaiwa kurudisha nyuma vita hivyo.

Post Comment