Highlights

Familia za wahasiriwa wa shambulizi la Manyatta Ginda wadai haki

Na Caroline Waforo

Familia za wahasiriwa wa shambulizi la hivi punde la wizi wa mifugo, katika eneo la Manyatta Ginda kaunti ndogo ya Marsabit Central, zimeitaka idara ya usalama jimboni kuhakikisha kuwa wahusika wote wa tukio hilo wanakamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria ili haki itendeke.

Wakizungumza leo Alhamisi baada ya kamati ya usalama pamoja na ile amani jimboni kuwatembelea na kuwasilisha rambirambi, familia hizo zimesisitiza haja ya usalama kuimarishwa.

Rambirambi hizo zimetolewa kwa familia ya afisa aliyeuawa wa akiba NPR katika eneo la Manyatta Ginda pamoja na mmiliki wa mifugo aliyeuawa katika tukio hilo, anayetoka katika eneo la Manyatta Wako Jaldesa.

Familia hizo pia zimeitaka idara ya usalama kuongeza idadi ya maafisa wa akiba NPR ili kudhibiti matukio ya mara kwa mara ya wizi wa mifugo.

Mwenyekiti wa kamati ya usalama jimboni na ambaye pia ni Kamishna wa kaunti James Kamau, amewataka wananchi kudumisha amani na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa muhimu.

Kwa upande wao, wanachama wa kamati ya amani wamesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na vyombo vya usalama katika kulinda amani, wakitahadharisha jamii dhidi ya kuwaficha wahalifu.

Doyo Galgallo, mwanachama wa kamati hiyo amesema kuwa usalama ni jukumu la kila mwanajamii.

Hapo jana Kamishna wa kaunti ya Marsabit James Kamau alithibitisha kuwa idara za usalama tayari zina majina ya washukiwa wa tukio hilo na juhudi za kuwasaka zinaendelea ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Post Comment