Highlights

Viongozi wa dini Marsabit walaani mauaji ya wizi wa mifugo, wataka Amani.

Na Samuel Kosgei

VIONGOZI wa kidini mjini Marsabit wameendelea kulaani tukio la hivi karibuni ambapo watu wanne walifariki dunia kufuatia jaribio la wizi wa mifugo katika eneo la Manyatta Ginda, eneo bunge la Saku, kaunti ya Marsabit.

Askofu wa Kanisa la Kianglikana (ACK) Dayosisi ya Marsabit, Qampicha Wario, amekashifu vikali tukio hilo akisema serikali inapaswa kuendeleza uchunguzi na kuwakamata wahalifu waliotoroka baada ya uvamizi huo, ambapo majangili wawili pia waliuawa.

Askofu Qampicha ametoa wito kwa jamii za Marsabit kuepuka kulipiza kisasi, akisisitiza kuwa si sahihi kuhusisha uhalifu na kabila fulani kwani ni vitendo vya watu binafsi.

Kwa upande wake, Imam wa Msikiti wa Jamia mjini Marsabit, Sheikh Mohamed Noor, amewataka wakazi kuendelea kudumisha amani ambayo imejengwa kwa muda mrefu. Aidha, ameihimiza idara ya polisi kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii.

Naye Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani kaunti ya Marsabit, Adan Chukulisa, amelaani tukio hilo na kuitaka serikali kuwachukulia hatua kali waliohusika. Amewahimiza wakazi wote kuendeleza uvumilivu na mshikamano.

Post Comment