Wakazi wa kaunti ya Marsabit kupata vitambulisho chini ya siku saba.
NA Nyabande Orwa
Katibu mkuu wa idara ya uhamiaji na huduma za uraia chini ya wizara ya usalama wa ndani na utawala wa kitaifa, Belio Kipsang, amesema muda wa kupata kitambulisho cha kitaifa katika kaunti ya Marsabit umepungua hadi takriban siku saba. Kipsang amesema hatua hiyo imetokana na matumizi ya teknolojia mpya katika ukusanyaji wa taarifa za raia.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuongoza kikao cha kuhamasisha machifu na manaibu chifu kuhusu umuhimu wa kuwaandikisha wananchi na kuelimisha jamii kuhusu ulazima wa kupata stakabadhi muhimu za kiserikali, ikiwemo vitambulisho vya kitaifa, vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo, Kipsang amesema zaidi ya watu 70,000 ambao bado hawajaandikishwa watafikiwa kwa wakati ufaao.
Kipsang alisema mpango wa kuhamasisha machifu kuongeza kasi ya usajili wa raia na kuanzisha vituo tamba vya usajili wa vitambulisho katika kaunti 15 za maeneo kame umetokana na changamoto za awali, ikiwemo mchakato wa kupigwa msasa na mtindo wa maisha ya kuhamahama wa wakazi. Amesema vituo hivyo vitaanza katika kaunti za Baringo, Turkana na West Pokot kabla ya kupanuliwa hadi kaunti nyingine 12.
Wakati huo huo, Katibu huyo amesema kutakuwa na vituo 12 vya kudumu katika kaunti ndogo kwa ajili ya usajili wa vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa Marsabit, hatua inayolenga kupunguza gharama na usumbufu kwa wakazi wa mashinani.
Aidha, Kipsang amewaonya machifu na maafisa wa serikali wanaodai au kutoza pesa kwa wananchi wanaotafuta vitambulisho, akisema watakabiliwa na hatua za kisheria kwa vitendo vya ufisadi.
Naye machifu wametoa wito kwa idara ya uhamiaji kuongeza idadi ya maafisa wa serikali wanaosajili wananchi katika maeneo ya mbali ya kaunti, ili kupunguza usumbufu na gharama kubwa wanazobeba wakazi wanaposafiri umbali mrefu kufuata huduma za usajili. Machifu wamesema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vitambulisho na stakabadhi nyingine muhimu za kiserikali.



Post Comment