Wakazi wa jimbo la Marsabit Wameshauriwa Kupanda Miti katika Msimu huu wa Mvua.
Na JB Nateleng
Wakazi wa Kaunti ya Marsabit County wametakiwa kuchangamkia msimu huu wa mvua kwa kuanza kupanda miti ili kusaidia kuafikia lengo la kupanda miti milioni 240 lililowekwa na serikali.
Akizungumza na kituo hiki ofisini mwake, Afisa Mkuu Msimamizi katika Idara ya Huduma za Misitu, Kenya Forest Service tawi la Marsabit, Kennedy Muthuri, amesema kuwa juhudi za upandaji miti katika kaunti hiyo zimekuwa zikiathiriwa na ukame unaoshuhudiwa mara kwa mara. Hivyo amewarai wakazi kutumia fursa ya mvua inayonyesha kwa sasa kupanda miti.
Muthuri amesema kuwa ili kufikia lengo la kupanda miti milioni 240 lililowekwa na serikali kuu, kila mwananchi anapaswa kupanda angalau miti 100 kila mwaka.
Aidha, Muthuri amesema kuwa mwaka jana walifanikiwa kupanda miti 24,000 katika eneo la karibu na Mount Marsabit, akibainisha kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na lengo la kaunti la kupanda miti milioni 24 kila mwaka.
Afisa huyo pia amewataka wafugaji wanaolisha mifugo yao ndani ya misitu kuiondoa mara moja ili kuepuka uchafuzi wa chemichemi za maji na kuruhusu mimea inayochipuka kukua vizuri



Post Comment