Wakazi wa Kargi, South Horr na Chalbi kuwasilisha kesi kortini kuhusu ongezeko la saratani
Na Nyabande Orwa
Wakazi wa maeneo ya Kargi, South Horr na Chalbi wanatarajiwa kuwasilisha kesi katika mahakama ya mazingira tarehe 30 mwezi huu wa Machi wakilalamikia kile wanachodai ni ongezeko la visa vya ugonjwa wa saratani katika maeneo hayo.
Akizungumza na kituo hiki mapema leo katika kipindi cha Amkia Jangwani, aliyekuwa mwakilishi wa wadi ya Kargi na ambaye pia yuko mstari wa mbele kupigania haki za wakazi kutokana na ongezeko hilo, Asunta Galgidele, amesema jamii hiyo hapo awali iliwasilisha kesi katika mahakama kuu ya Nairobi. Hata hivyo waliagizwa kuipeleka kesi hiyo katika Mahakama ya mazingira na ardhi iliyoko mjini Isiolo.
Asunta amesema kuwa suala la saratani ya koo katika eneo hilo lilianza kuibuliwa kwa nguvu mwaka wa 2007 baada ya watu wanane kufariki kutokana na ugonjwa huo, hali iliyochochea juhudi za kutaka kubaini chanzo chake.
Kwa upande wake, Hilary Alkano, mkazi wa eneo hilo na mwanaharakati wa haki za mazingira, anadai kuwa kuna taka hatari zilizoachwa katika eneo hilo miaka ya 2000. Anasema serikali pamoja na viongozi wa kisiasa wamekuwa kimya kuhusu madai hayo. Pia anasema juhudi zao za kupata majibu kutoka kwa maafisa wa serikali wanaochunguza maji ya visima vya eneo hilo bado hazijazaa matunda.
hata hivyo, muuguzi wa saratani katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo, Joyce Mukoro, anawashauri wakazi wa maeneo yaliyoathirika kutafuta uchunguzi na matibabu mapema wanapoanza kuona dalili za ugonjwa huo ili kupunguza madhara.



Post Comment