Highlights

Mashindano ya michezo ya muhula wa kwanza yaanza Marsabit Central.

Na JB Nateleng

Mashindano ya michezo ya muhula wa kwanza katika ngazi ya kaunti yameanza rasmi leo katika eneo la Marsabit ya kati.

Mashindano hayo yanahusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha, raga, handiboli, kurusha mkuki na basketboli. Shule zote zilizoshinda katika mashindano ya kaunti ndogo kote jimboni ndizo zinazoshiriki.

Katika mchezo wa raga, shule ya upili ya mseto ya Marsabit imefanikiwa kutetea ubingwa wake baada ya kuilaza shule ya upili ya wavulana ya Chalbi kwa alama 60 kwa 0. Ushindi huo unaifanya shule hiyo kuwakilisha kaunti ya Marsabit katika mashindano ya kanda yatakayofanyika Meru wiki ijayo.

Katika mashindano ya kurusha mkuki, Rob Debano kutoka Marsabit Central aliibuka mshindi baada ya kurusha umbali wa mita 69.50. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Rob Miyo kutoka Sololo kwa mita 61.80, huku Galgallo Guyo akishika nafasi ya tatu kwa mita 60.36.

Kwa upande wa riadha ya wasichana, Adho Mamo kutoka Marsabit Central alishinda mbio za mita 10,000. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Sarah Naramat kutoka Loiyangalani, huku Midina Adano wa Chalbi na Rose Lepurski wa Marsabit Central wakimaliza katika nafasi ya tatu na nne mtawalia.

Kwa upande wa wavulana, Suleiman Hussein kutoka Moyale alishinda mbio za mita 10,000. Hussein Abdikadir kutoka Marsabit Central alishika nafasi ya pili, huku Abdinur Abdullahi kutoka Moyale akimaliza katika nafasi ya tatu.

Wakati huo huo, mbio za mita 400 zilianza leo na fainali zake zinatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa.

Post Comment