Familia moja Loglogo yaomba msaada wa matibabu kwa mtoto mwenye ugonjwa wa Recto-Vagina Fistula,
Na Caroline Waforo.
Familia moja kutoka eneo la Loglogo eneobunge la Laisamis Kaunti ya Marsabit imejitokeza kuomba msaada wa matibabu kwa mtoto wao wa kike wa umri wa miaka 13 anayeugua ugonjwa wa Recto-Vagina Fistula hali ianyomfanya kushindwa kuzuia mkojo na kinyesi.
Msichana huyo Fecha Esyimfecha amekuwa akiugua ugonjwa huo tangu kuzaliwa kwake hali ambayo imeathiri pakubwa maisha yake ya kila siku na kumzuia kuishi kama mtoto mwingine wa ria lake.
Akizungumza na wanahabari nyumbani kwao leo Alhmisi mamake Arbe, Hiroya Orre amesema binti yake amelazimika kutumia nepi muda wote huku akieleza kuwa familia imelemewa na gharama za matibabu.
Hiroye ameongeza kuwa licha ya mwanawe wa gredi ya 4 katika shule ya msingi ya Muslim Primary kuwa mwanafunzi mwerevu, anakabiliana na unyanyapaa kutoka kwa wanafunzi wenzake hali inayotatiza masomo yake.
Kwa upande wa babake Fecha, mzee Martin Esyimfecha mwenye umri wa miaka 50 familia tayari imetumia zaidi ya shilingi 600,000 kwa matibabu ya binti yao ambaye hadi kufikia sasa amefanyiwa upasuaji mara mbili katika hospitali ya Kijabe.
Ameongeza kuwa Arbe alipaswa kurejea hospitalini mwezi Aprili mwaka jana ila hilo halikuwezekana kutokana na ukosefu wa fedha.
Mzee Esyimfecha ametoa wito kwa Rais William Ruto, viongozi wa jimbo hili pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kote nchini kujitokeza na kumsaidia mwanawe aweze kupate matibabu.
Wito huu pia umetolewa na baadhi ya wanakijiji akiwemo Diboya Idris pamoja na Musa Lepurkei ambao wamekuwa wakiisaidia familia hii kumtafutia msichana huyo matibabu.



Post Comment