Highlights

Waumini wa Kiislamu wahimizwa kuwasaidia wasiojiweza

Na JB Nateleng

Leo ikiwa ni Ijumaa ya mwisho katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, waumini wa Kiislamu wametakiwa kujitokeza kuwasaidia watu wasiojiweza katika jamii.

Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya simu, Sheikh wa Msikiti wa Jamia mjini Marsabit, Sheikh Mohamed Noor, amesema kuwa Ijumaa hii ya mwisho ya Ramadhani ina umuhimu wa kipekee, hasa katika kuonyesha huruma na kuwajali wale wenye mahitaji maalum.

Sheikh Noor amesema ni wajibu wa kila muumini kuhakikisha anatenda mema yanayoweza kuboresha maisha ya wanajamii, akiongeza kuwa baraka hupatikana kupitia kile mtu anachotoa kwa moyo wa ukarimu.

Aidha, amewahimiza wananchi kusaidiana bila ubaguzi wa dini, tabaka, rangi au mahali wanapotoka, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza njaa na changamoto nyingine zinazozikumba baadhi ya familia katika jamii.

Wakati huo huo, Sheikh Noor amewataka wakazi wa Marsabit kuendelea kudumisha amani na mshikamano wakati huu wa Ramadhani na hata baada ya mwezi huo mtukufu kumalizika.

Mwezi wa Ramadhani unatarajiwa kumalizika wiki ijayo, Alhamisi au Ijumaa, kulingana na muonekano wa mwezi. Hapo ndipo waumini wa Kiislamu watakaposherehekea sikukuu ya Idi.

Post Comment