Vijana wahimizwa kuongoza juhudi za utunzaji mazingira Loiyangalani
Na JB Nateleng
Wakazi wa Loiyangalani wamehimizwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulinda na kuboresha mazingira, wakikumbushwa kuwa mazingira safi na salama ni haki ya kila mwananchi.
Mwanamazingira Emmanuel Emanman, almaarufu UB-40, amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika shughuli za utunzaji wa mazingira katika eneo la Loiyangalani. Amesema kuwa hatua hiyo inahitaji uwajibikaji, ukomavu na moyo wa kujitolea ili kuhakikisha jamii inaishi katika mazingira safi na salama.
Aidha, amewahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kulinda mazingira, zikiwemo kudumisha usafi na kutunza rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesisitiza kuwa juhudi kama hizo ni muhimu katika kuhakikisha Loiyangalani inaendelea kuwa na mazingira bora kwa wakazi wake.
Emanman alitoa kauli hiyo baada ya kushiriki katika zoezi la kusafisha taka na uchafu uliokuwa umeziba mfereji wa Kulapesa, uliokuwa ukizuia maji kupita kwa urahisi katika eneo la Loiyangalani, kaunti ya Marsabit.



Post Comment