Highlights

Mwavuli wa Maikona VSLA waanzishwa kuimarisha biashara za wanachama

Na Caroline Waforo

Vikundi 40 vya kijamii vya akiba na mikopo kutoka wadi ya Maikona eneobunge la North Horr kaunti ya Marsabit vimeungana na kuunda mwavuli mmoja unaojulikana kama Maikona Village Savings and Loan Associations katika hatua inayolenga kuviwezesha vikundi hivyo kiuchumi.

Hatua hiyo imewezeshwa kupitia ushirikiano wa mashirika mbalimbali yakiwemo Mercy Corps, PACIDA, Life and Peace Institute kwa kushirikisha pia serikali kuu na ile ya kaunti ya Marsabit chini ya mradi wa RANGE.

Mradi huo wa RANGE unaoendeshwa na Mercy Corps na kutekelezwa kwa ushirikiano na mashirika mengine katika kaunti za Marsabit, Isiolo na Samburu umefadhiliwa na ubalozi wa Uholanzi kwa lengo la kuimarisha ustahimilivu wa jamii zinazoishi katika maeneo kame na nusu kame ili kuchangia katika maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Katika mkutano uliofanyika Jumamosi katika bustani ya Baraza iliyoko wadi ya Maikona, wanachama wa vikundi hivyo ambao ni akina mama, walipata nafasi ya kuonyesha biashara zao na kubadilishana mawazo kibiashara.

Akizungumza na Shajara afisa kutoka shirika la Mercy Corps Joy Sariyon amesema kuundwa kwa mwavuli huo kutawapa wanachama nafasi ya kuimarisha usimamizi wa fedha, kuunganishwa na taasisi za kibinafsi pamoja na masoko ya bidhaa zao.

Kwa upande wake afisa kutoka shirika la PACIDA Guyo Boru amesema kuwa kupitia mwavuli huo wanachama hao kutoka lokesheni zote za wadi ya Maikona watapata nafasi ya kupanua biashara zao.

Wanufaika wa mpango huu wakiongozwa na Dokesa Ali wamepongeza mashirika yaliyowaleta pamoja wakisema kuwa hatua hiyo itawawezesha kupata mikopo ya kukuza biashara zao na pia kukithi mahitaji yao ya kifedha hasa wakati wa dharura.

Hatua hii imepongezwa na Mratibu wa Idara ya Huduma za Jamii katika kaunti ya Marsabit Vincent Musee, ambaye amesema kuwa wanachama hao watanufaika pakubwa kupitia elimu ya kifedha huku akisema kuwa baada ya kukamilika kwa mikakati yote kundi hilo litasajiliwa rasmi.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkrugenzi wa Idara ya biashara katika kaunti ya Marsabit Hussein Kasa amesema kuundwa kwa mwavuli huo kutawafungulia wafanyibiashara hao fursa zaidi ndani na nje ya kaunti ya Marsabit.

Wakati wa hafla hiyo wanachama wa vikundi hivyo walipata mafunzo ya kifedha kutoka kwa benki ya Equity pamoja na taasisi ya Solution Sacco.

Aidha, mashirika ya kibinafsi kama SIDAI Africa yalishiriki katika hafla hiyo na yanatarajiwa kutoa huduma mbalimbali zinazoweza kusaidia mwavuli wa Maikona VSLA kukuza na kuimarisha biashara za wanachama wake.

Post Comment