Raia wa Poland apigwa faini ya shilingi 20,000 kwa kupatikana na bangi Marsabit.
Na Nyabande Orwa
Raia wa Poland mwenye umri wa miaka 47 aliyekamatwa na misokoto 24 ya bangi siku ya Jumatano katika eneo la Stage 45, amepigwa faini ya shilingi elfu ishirini na mahakama ya Marsabit baada ya kukiri mashtaka.
Mwanaume huyo anayejulikana kama Dariusz Rafal alifika mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Marsabit, Edward Oboge, ambapo alikiri kosa hilo na kutozwa faini ya shilingi 20,000.
Baada ya kulipa faini hiyo, Rafal aliachiliwa huru baada ya kuwa kukesha korokoroni usiku mmoja.
Akithibitisha tukio hilo, OCPD wa Marsabit Central Beethoven Gachago alisema mshukiwa huyo alikamatwa baada ya raia kutoa taarifa kwa polisi walipomwona akiwagawia vijana bangi katika kituo hicho cha magari.
Gachago aliwapongeza raia kwa kushirikiana na polisi katika juhudi za kupambana na matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya katika eneo la Marsabit.



Post Comment