Highlights

Visa vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) vyatajwa kupungua Marsabit.

Na JB Nateleng

Huku dunia ikiadhimisha siku ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) leo Jumanne, visa vya ugonjwa huo vimetajwa kupungua kaunti ya Marsabit ambapo visa 710 vilirekodiwa mwaka wa 2025, asilimia 8 ya visa hivyo ikiwa miongoni mwa watoto.

Akizungumza na idhaa hii, Msimamizi Mkuu wa masuala ya kifua kikuu katika kaunti ya Marsabit, Sori Gone, amesema kuwa visa vya ugonjwa huo vilipungua kutokana na mikakati iliyowekwa na Idara ya Afya, hasa katika maeneo ya mpakani kati ya Kenya na Ethiopia.

Ameeleza kuwa kaunti ndogo ya Moyale iliongoza kwa idadi ya visa ikiwa na 326, ambapo 35 ni watoto. Eneo hilo pia liliripoti visa viwili vya kifua kikuu sugu kwa dawa (DR-TB).

Kaunti ndogo ya Saku ilirekodi visa 193 vya TB, ambapo 13 ni watoto, pamoja na visa viwili vya DR-TB.

Katika eneo bunge la Laisamis, jumla ya visa 117 viliripotiwa, saba kati yake ni vya watoto, huku hakukuwa na kisa chochote cha TB sugu kwa dawa.

Nalo eneo bunge la North Horr lilirekodi visa 64, kimoja kikiwa ni cha mtoto.

Sori ameongeza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2026, eneo la Moyale bado linaongoza kwa visa vya kifua kikuu huku akisema hali hii inachangiwa na jiografia ya eneo hilo kuwa mpakani, hata hivo juhudi za kudhibiti zinaendelea kuimarishwa.

Aidha, ametoa wito kwa wakazi wa Marsabit kuacha unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa kifua kikuu, akisisitiza kuwa ugonjwa huo unatibika na dawa zake hutolewa bila malipo.

Post Comment