Highlights

Ukosefu wa ushahidi watajwa kuangusha kesi za dhuluma Marsabit.

Mashahidi kutoka upande wa waathiriwa wanapaswa kujitokeza mahakamani ili kusaidia upatikanaji wa haki katika kesi za dhuluma na ukiukaji wa haki za binadamu. Hayo ni kwa mujibu wa mtetezi wa haki za binadamu katika kaunti ya Marsabit, Nuria Golo.

Akizungumza na Radio Jangwani, Nuria amesema kuwa licha ya kuwepo kwa visa vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu katika kaunti hii, ni kesi chache zinazofaulu mahakamani huku nyingi zikitupiliwa mbali kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wakazi wa Marsabit kuwa na ujasiri wa kufika mahakamani na kutoa ushahidi, hasa katika kesi za dhuluma za kingono dhidi ya watoto.

Nuria amesema changamoto nyingine zinazochangia kushindwa kwa kesi hizo ni pamoja na ukosefu wa ufahamu wa sheria miongoni mwa wananchi, kiwango cha chini cha elimu, pamoja na kutofahamu lugha ya taifa.

Aidha, amesema kuwa wakati mwingine baadhi ya familia hukubaliana kutoa ushahidi wa uongo ili kuficha ukweli, jambo linalozorotesha juhudi za kupata haki kwa waathiriwa.

Post Comment