Highlights

Serikali yahamasisha matumizi ya nishati safi kupitia mradi wa KOSAP

Na Nyabande Orwa

Kama njia moja ya kuhakikisha mazingira ya kaunti hii yanalindwa na kuboreshwa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, serikali kuu kwa kushirikiana na serikali ya kaunti ya Marsabit zimebuni mbinu mbadala za kuwasaidia wananchi kupata nishati safi kwa matumizi ya nyumbani.

Hayo ni kulingana na afisa kutoka wizara ya nishati anayehusika na mradi wa KOSAP katika kaunti hii, Gideon Jalle.

Akizungumza na kituo hiki mapema leo katika kipindi cha Amkia Jangwani, Jalle amesema ushirikiano huo unalenga kuhamasisha matumizi ya nishati ya sola katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme, badala ya kutumia jenereta. Aidha, matumizi ya majiko yanayotoa hewa chafu kidogo yanahimizwa ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakati huo huo, Jalle amesema kuwa katika kaunti 14 ambako mradi huu unatekelezwa, maafisa wa kaunti wanapatiwa mafunzo na ujuzi ili kuhakikisha wanaendeleza juhudi za mradi wa KOSAP hata baada ya wafadhili kuondoka.

Vilevile, amesema kuwa kupitia matumizi ya majiko yanayotunza mazingira, wanafunzi wanapata muda zaidi wa kuwa darasani kwani hawalazimiki tena kwenda kutafuta kuni. Pia, magonjwa yanayotokana na moshi yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Jalle amewahimiza wakazi wa kaunti hii kukumbatia bidhaa za KOSAP ili kuboresha mazingira na maisha ya familia zao.

Post Comment