Serikali kuu na kaunti ya Marsabit zashirikiana kukabiliana na ukame
NA Nyabande Orwa
Serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Marsabit zimeanza mikakati ya pamoja ya kukabiliana na athari za ukame unaoendelea katika kaunti hii.
Hayo yamesemwa na afisa mkuu mtendaji wa idara ya mifugo na kilimo kaunti ya Marsabit, Tache Elema Duba. Akizungumza kwa simu na kituo hiki, Duba amesema ushirikiano huo umeleta pamoja washikadau mbalimbali ili kujadili namna ya kuwasaidia wananchi, hasa waliokumbwa zaidi na athari za ukame, pamoja na kutathmini idadi ya familia na mifugo iliyoathirika.
Elema amesema kupitia mpango huo, wafugaji walioathirika zaidi watapokea chakula cha mifugo na maji. Aidha, wafugaji pia wananufaika na mpango wa serikali kuu wa Inua Jamii unaolenga wakazi wa maeneo kame. Ameongeza kuwa kuna magonjwa yanayoathiri ngamia, hali ambayo serikali ya kaunti inaikabili kupitia chanjo.
Hata hivyo, baadhi ya wafugaji wanasema licha ya mvua chache zilizonyesha katika msimu wa Oktoba, Novemba na Disemba mwaka jana, maeneo kadhaa bado yako katika hatua ya tahadhari kutokana na upungufu wa nyasi. Kutokana na hali hiyo, mifugo imeanza kudhoofika kwa kukosa malisho.
Tumal Orto, mfugaji kutoka eneo la Maikona, amesema mifugo midogo kama mbuzi na kondoo inapitia wakati mgumu.
Orto ametoa wito kwa serikali na mashirika mengine kuingilia kati mapema ili kuzuia janga kama lililotokea mwaka 2022. Pia amewahimiza wafugaji kuanza kuuza mifugo yao mapema kabla hali haijazidi kuwa mbaya ili wapate soko bora.



Post Comment