Highlights

Mahakama yatangaza rasmi kifo cha mfanyabiashara wa Marsabit Kunni Hele Halanka aliyetoweka mwaka 2022

Mahakama kuu ya Marsabit imemtangaza rasmi mfanyabiashara Kunni Hele Halanka kuwa amefariki dunia karibu miaka minne tangu alipodaiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana jijini Nairobi.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa na umri wa miaka 70, alitoweka tarehe 7 mwezi Februari mwaka 2022 baada ya kuripotiwa kutekwa nyara akiwa ndani teksi alipokuwa akielekea nyumbani kwake kutoka hoteli ya Weston jijini Nairobi.

Licha ya vyombo vya usalama kusema kuwa vilikuwa vinachunguza kisa hicho Kunni hajawahi kupatikana wala kuwasiliana na familia yake, hali iliyoiweka familia katika hali ya sintofahamu kwa muda mrefu.

Katika uamuzi uliotolewa Januari tarehe 16 mwaka huu, mahakama ilieleza kuwa mazingira ya kutoweka kwa Kunni Hele yalionyesha wazi kuwa hakuna uwekezano wa kupatikana akiwa hai.

Uamuzi huo ni kufuatia ombi la tarehe 11 mwezi Disemba mwaka 2025 lililowasilishwa na mwanawe Alex Ali Kunni kwa niaba ya familia akiambatanisha idhini ya wanafamilia wote.

Kwa mujibu wa kifungu cha 118A cha Sheria ya Ushahidi mtu anaweza kutangazwa kuwa amefariki iwapo hajulikani alipo kwa kipindi wa miaka saba.

Hata hivyo sheria hiyo inaruhusu mahakama kutoa uamuzi huo mapema endapo mazingira ya kutoweka yanadhihirisha wazi kuwa hakuna matumaini ya mtu huyo kupatikana akiwa hai.

Kufuatia uamuzi huo familia sasa itaweza kupata cheti cha kifo na kusimamia mali zake kisheria.

Itakumbukwa kuwa mfanyabiashara Roba Abduba Sereka pia alidaiwa kutekwa nyara mwaka huo wa 2022 katika eneo la Green Valley jijini Nairobi na hajulakani aliko hadi kufikia sasa.

Post Comment