Kipsang awataka machifu kuhakikisha wanafunzi wako shuleni.
NA Nyabande Orwa
Katibu mkuu wa idara ya uhamiaji na huduma za uraia, Belio Kipsang, amewataka machifu kuhakikisha wanatekeleza agizo la serikali la kuhakikisha watoto wote wanaofaa kuwa shuleni wanahudhuria masomo.
Akizungumza katika Kaunti ya Marsabit wakati wa kikao na machifu, Kipsang amesema kuwa kutimiza agizo hilo kutasaidia serikali kufikia malengo yake katika sekta ya elimu na kulinda haki ya kila mtoto kupata elimu, hasa wakati huu ambapo wanafunzi wa Gredi ya 10 wanaanza masomo.
Mbali na hilo, Kipsang amewataka machifu kushirikiana na vyombo vya usalama katika kupambana na matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya katika jamii.
Wito huo umeungwa mkono na kamishna wa kaunti ya Marsabit, James Kamau, aliyeahidi kushirikiana kwa karibu na machifu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanarejea shuleni kikamilifu.
Hata hivyo, Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Loiyangalani, Stanley Kimanga, anasema kuwa licha ya juhudi za serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea shuleni, eneo hilo linakumbwa na changamoto za ukame, umaskini na umbali mrefu wa makazi.
Ameongeza kuwa wanafunzi wengi hutegemea chakula cha msaada shuleni, hali inayowahamasisha kuendelea na masomo. Kimanga anasema serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali inaendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu.



Post Comment