Loading Now

Highlights

Jamii za Marsabit zahimizwa kukomesha ubaguzi dhidi ya makundi maalum

Na JB Nateleng

Wananchi katika kaunti ya Marsabit wamahimizwa kukomesha ubaguzi dhidi ya makundi maalum na kuheshimu haki za kila mmoja bila kujali jinsia, kabila, dini, hali ya kiafya au hadhi ya kijamii.

Akizungumza na idhaa hii kwa njia ya kipekee, Mkurugenzi wa shirika la Marsabit Women Advocacy and Development Organization (MWADO) Nuria Gollo, amesema kuwa jamii za Marsabit bado hazijakumbatia kikamilifu suala la usawa, hali inayochangia kuendelea kwa visa vya kutengwa kwa baadhi ya watu.

Nuria ameeleza kuwa bado makundi maalum katika jamii kama vile watu wanaoishi na ulemavu pamoja na wanaoishi na virusi vya UKIMWI, wanakabiliwa na unyanyapaa akisisitiza haja ya jamii kukomesha hulka hiyo.

Nuria amesisitiza kuwa ubaguzi huo unapelekea watoto hasa wa kike wanaodhulumiwa kukosa kuripoti visa hivyo kwa idara husika kwa hofu ya kutengwa.

Na kuhusu masuala ya uongozi Nuria ameitaka serikali kuu pamoja na ile ya kaunti kuwajumuisha wanawake, vijana na makundi mengine maalum kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.

Kadhalika, ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kuongeza juhudi za kuhamasisha umma kuhusu madhara ya ubaguzi katika jamii za wafugaji, ili kuimarisha mshikamano na kuishi kwa amani.

Post Comment