Highlights

Gachagua asutwa vikali na viongozi wa kenya kwanza kwa matamshi yake dhidi ya viongozi wa kaskazini mwa nchi

NA JB Nateleng

Rigathi Gachagua asutwa vikali na viongozi wa Kenya kwanza kwa matamshi yake dhidi ya viongozi wa Kaskazini mwa nchi

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la seneti Aaron Cheruiyot amemsuta vikali aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua kufuatia matamshi yake ya hivi maajuzi kuwa viongozi wa Kaskazini mwa nchi wametelekeza maeneo yao na kuwekeza jijini Nairobi.

Akizungumza leo Jumamosi katika hafla ya kuyawezesha makundi 21 ya akina mama wa Qirta Qorma kutoka Saku, Cheruiyot amesema kwamba eneo la Kaskazini lilikuwa limetengwa tangu Kenya ilipopata uhuru wake huku akidai kwamba serekali ya Kenya Kwanza inajizatiti kuhakikisha kwamba wakenya walio Kaskazini mwa Kenya wanahudumiwa na kupewa maendeleo kama wakenya walioko katika maeneo mengine.

Kadhalika Cheruiyot ametoa wito kwa wakaazi wa Marsabit kuzidi kudumisha amani ili kupata maendeleo.

Kauli sawia imekaririwa na msaidizi wa kibinafsi wa Rais William Ruto, Farouk Kibet ambaye amewataka wakazi wa Marsabit kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kuongoza taifa kwa muhula wa pili.

Kibet amewasuta wapinzani wa rais Ruto kwa kueneza siasa duni za kikabila.

Kimani Ichungwah ambaye ni kiongozi wa walio wengi katika bunge la Kitaifa amesifia hatua na juhudi za Rais William Ruto ya kuboresha miundo mbinu ya nchi.

Hafla hiyo imehudhuria na viongozi mbalimbali akiwemo mbunge wa Kibwezi Mwengi Mutuse, mbunge wa Taveta John Bwire kati ya viongozi wengine.

Post Comment