Local Bulletins

Waokaje wa mikate waonywa dhidi ya kupunguza uzani na kutoa matangazo ya uwongo

Silvio Nangori

Mamlaka ya kuthibiti Mashindano katika Biashara nchini imwaagiza waokaji wa mikate kukoma kuwaibia wakenya.

Kwenye taarifa yake hii leo Mamlaka hiyo imewaagiza wote wanaotengeneza mikate kuweka bayana taarifa yote muhimu katika uuzaji wa mikate yao.

Mamlaka hiyo imewataka waokaji wa mikate kuweka wazi tarehe ya kutengenezwa kwa mikate na tarehe ambayo mikate hiyo inatarajiwa kuharibika.

Kulingana na uchunguzi wake mikate mingi imekosa kuweka wazi tarehe ya kuokwa na badala yake kuandikwa tu kwamba ni nzuri kabla ya tarehe Fulani.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Wang’ombe Kariuki amesema kwamba haki za watumiaji inakiukwa wakati taarifa muhimu inakosa kuwekwa wazi.

Uchunguzi wa mamlaka hiyo umeonyesha kuwa kampuni nyingi za kuoka mikate zimetangaza mikate yao kuwa na virutubishi Fulani kama maziwa na virutubishi vingine ambavyo haviko.

Vile vile imesema kwamba baadhi ya wazalishaji wamefeli kuonyesha kiasi cha mikate wanayozalisha huku wengine wakiishia kuwadanganya watumiaji kwa vifaa walizotumia katika kuoka mikate.

Mamlaka hiyo imeonya kuwa itaendelea kufanya ukaguzi wake mara kwa mara kwenye bidhaa mbali mbali nchini na wale watakaopatikana kukiuka maagizo ya serikali watakabiliwa kisheria.

Haya yanajiri wakati ambapo wakenya wengi wanalalama kwamba mikate wanayonunua siku hizi haina uzito unaofaa au hata inachina mapema.

Subscribe to eNewsletter