Highlights

Watu wawili wahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la mauaji, Marsabit

Watu wawili walioshtakiwa katika mahakama kuu ya Marsabit kwa kutekeleza mauaji ya kijana mmoja kutokana na mzozo wa shilingi 100 katika lokesheni ya Manyatta Jillo, kaunti ndogo ya Marsabit Central wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.

Wawili hao Bonaya Abkula na Halakhu Dida wamepewa hukumu hiyo baada ya kupatikana na kosa la kumpiga na kumsababishia kifo marehemu Guyo Jaldesa mnamo tarehe 13 mwezi Septemba mwaka 2024.

Mahakama ilielezwa kuwa mshukiwa wa kwanza alimvamia marehemu kwa fimbo huku mshukiwa wa pili akimpiga kwa mikono na mateke walipokuwa wakidai shilingi 100 alizodaiwa kuchukua.

Marehemu alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata.

Akitoa hukumu hiyo leo Alhamisi, Jaji wa mahakama kuu ya Marsabit Francis Rayola ametahadharisha jamii dhidi ya kuchukua hatua mikononi mwao.

Wawili hao wana siku 14 kukata rufaa.

Wakati uou huo

Mwanaume mmoja wa umri wa makamo amepigwa faini ya shilingi 100,000 au kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kupatikana na makosa mawili yanayofungamana na tuhuma za wizi katika lokesheni ya Mountain kaunti ndogo ya Marsabit Central.

Katika shtaka la kwanza hakimu mkaazi wa mahakama ya Marsabit Edward Oboge amempata na hatia Abdikadir Mohammed Wabera almaarufu Dabaso kwa kutekeleza wizi wa nguo ya thamani ya shilingi 25,000 pamoja na bidhaa mbali mbali za mapambo zenye thamani ya shilingi 250,000 kwa ushirikiano na watu wengine mnamo tarehe 19 mwezi Agosti 2025.

Katika shtaka la pili mhukumiwa amepatikana na kosa la kupatikana na bidhaa za mapambo zilizoshukiwa kuwa za wizi mnamo tarehe 23 Agosti.

Post Comment