Wanafunzi wa gredi ya tisa wabuni roboti ya kuimarisha kilimo, Marsabit
Na JB Nateleng
Ubunifu umechukua nafasi ya kipekee katika kaunti ya Marsabit baada ya wanafunzi wa gredi ya tisa kutoka shule ya msingi ya Marsabit EAPC Child Development Centre kubuni roboti ya kilimo inayolenga kuimarisha uzalishaji wa chakula katika eneo hili.
Wanafunzi hao Jackline Sarafina, Austine, Elimlim na Fardosa Shukri wanasema roboti hiyo imeundwa kusaidia wakulima katika kupima unyevunyevu wa udongo, kupanda mbegu kwa mistari iliyo dhabiti, kunyunyizia dawa kwa usahihi, pamoja na kufuatilia ukuaji wa mazao.
Ubunifu huo unakuja wakati ambapo wakulima kutoka Marsabit wanakabiliwa na changamoto za mavuno duni kutokana na ukame.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, teknolojia hiyo itasaidia kuongeza tija, kupunguza upotevu wa rasilimali na kuhamasisha kilimo cha kisasa.
Wanafunzi hao sasa wanatafuta usaidizi kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuboresha roboti hiyo kwa manufaa ya wakulima wadogo kote kaunti ya Marsabit.
Joseph Diba, mshirikishi wa shirika la Compassion International, amepongeza ubunifu huo akisema ni ushahidi kwamba vijana wa Marsabit wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika jamii.
Amesema roboti hiyo ya kilimo ni wazo la kipekee linaloweza kubadilisha taswira ya uzalishaji wa chakula katika maeneo kame.
Aidha, Diba amewahimiza walimu wakuu pamoja na Idara ya elimu katika Kaunti ya Marsabit kuiga mfano huo kwa kuunganisha ubunifu na teknolojia katika utekelezwaji wa mtaala wa umilisi (CBC).



Post Comment