Loading Now

Highlights

Walimu Marsabit walalamikia huduma za matibabu chini ya SHA

Na Nyabande Orwa

Serikali inatafuta suluhu ya mvutano uliopo kati ya walimu na bima ya afya ya jamii, Social Health Authority (SHA), kuhusu huduma za matibabu wanazopata walimu.
Waziri wa afya Aden Duale, pamoja na tume ya kuwaajiri walimu nchini (TSC) na viongozi wa chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya anuwai  (KUPPET), wanatarajiwa kufanya kikao kesho jijini Nairobi kujadili suala hilo.

Hatua hii inajiri saa chache baada ya katibu mkuu wa KUPPET tawi la Marsabit, Sarr Galgalo, kutoa wito kwa wasimamizi wa SHA mjini Marsabit kuingilia kati na kutatua changamoto wanazokumbana nazo walimu wanapotafuta huduma za matibabu katika hospitali zinazotoa huduma za bima hiyo.

Akizungumza na kituo hiki ofisini mwake, Galgalo amesema kabla ya walimu kuhamia kwenye bima hiyo, walipewa uhakikisho kwamba wangepata huduma bora zaidi ikilinganishwa na zile walizokuwa wakipata kupitia bima za kibinafsi.

Hata hivyo, anasema baadhi ya walimu wamelazimika kurudishwa nyumbani kutokana na kukosa huduma katika hospitali hizo.

Katibu huyo sasa anatoa wito kwa idara husika kuchukua hatua za haraka ili kutatua tatizo hilo.

Wakati huo huo, Galgalo ameitaka serikali kuhakikisha kuwa miundombinu ya kutosha inapelekwa katika shule za maeneo ya mashinani pamoja na vifaa vya kujifunzia, ili kusaidia utekelezaji wa mtaala wa CBC.

Post Comment