Wafugaji wametakiwa kukumbatia uongozi wa wanawake kwa manufaa ya kujenga jamii imara na yenye maendeleo.
Na JB Nateleng
Jamii ya wafugaji imetakiwa kukumbatia uongozi wa wanawake kwa manufaa ya kujenga jamii imara na yenye maendeleo.
Akizungumza jana katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika katika eneo la Gadamoji, eneo bunge la Saku, Kaunti ya Marsabit, Mwenyekiti wa Indigenous Women Council ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Isiolo Gender Watch, Grace Lolim, amesema kuwa huu ni wakati mwafaka kwa jamii kuwapa wanawake nafasi ya kuongoza kwa sababau wanawake wana uzoefu na uwezo unaoweza kusaidia kuleta maendeleo katika jamii.
Aidha ameeleza kuwa akina mama tayari wameonyesha uwezo wao wa kuongoza, akitaja baadhi ya kaunti zinazoongozwa na wanawake nchini kuwa zimeweza kushuhudia maendeleo makubwa huku akiitaka jamii ya wafugaji katika maeneo ya kaskazini mwa nchi kukumbatia uongozi wa wanawake.
Grace pia ametoa wito kwa vijana na wazee kutokubali kutumika kuwashambulia wanawake wanaotafuta nafasi za uongozi, akisema kuwa hii ni mila na tamaduni zilizopitwa na wakati.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mkurugenzi wa shirika la Marsabit Women Advocacy Development Organization (MWADO), Nuria Gollo, ambaye amewataka wanawake kuwaunga mkono wenzao wanaotafuta nafasi za uongozi ili kuleta mabadiliko ambayo jamii imekuwa ikisubiri kwa muda mrefu.



Post Comment