Ukame waathiri watoto na wazee Laisamis, Marsabit
NA Nyabande Orwa
Watoto walio chini ya miaka mitano pamoja na wazee wanaendelea kuathirika pakubwa na hali ya ukame katika wadi za Kargi kusini na Loiyangalani eneo bunge la Laisamis, kaunti ya Marsabit.
Kwa mujibu wa msimamizi wa afya katika eneo bunge la Laisamis, Yusuf Galmogle, kiwango cha utapiamlo miongoni mwa watoto kwa sasa kimesimama katika asilimia 16.2, hali ambayo anasema huenda ikaongezeka kadri siku zinavyosonga.
Akizungumza na kituo hiki, Galmogle amesema familia nyingi zimehama makazi yao wakisonga msituni kuwatafutia mifugo lishe, jambo linalowaacha watoto na wazee katika hatari kubwa ya njaa. Amesisitiza haja ya wahisani na washikadau kujitokeza kutoa msaada wa haraka ili kudhibiti hali hiyo.
Wakati huo huo, Chifu wa eneo la Loglogo, Andrew Korolle, amesema kupungua kwa ufadhili kutoka kwa wahisani kumeongeza makali ya ukame, hasa kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Chifu Korolle ameongeza kuwa ukame umeathiri pia uchumi wa jamii, akisema bei ya mifugo imeshuka kwa kiwango kikubwa na kuacha familia nyingi katika hali ya umasikini.



Post Comment