Raia wa Poland anaswa na misokoto 24 inayoshukiwa kuwa bangi mjini Marsabit
Na Caroline Waforo
Mwanaume mmoja raia wa Poland amekamatwa na maafisa wa polisi akiwa na misokoto 24 inayoshukiwa kuwa bangi hapa mjini Marsabit.
Akithibitisha kisa hicho cha leo Jumatano, OCPD wa Marsabit Central Beethoven Gachago, amesema kuwa mwanaume huyo alikamatwa kufuatia taarifa zilizotolewa na wananchi waliodai kuwa mshukiwa alikuwa akisambaza misokoto inayoshukiwa kuwa bangi katika stendi ya bodaboda ya Stage 45.
Gachago amesema kuwa maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria mjini, walifanya upekuzi katika gari la mshukiwa na kufanikiwa kupata misokoto hiyo.
Kwa mujibu wa OCPD Gachago raia huyo wa Poland na ambaye ni mtalii aliingia nchini tarehe 13 mwezi Februari mwaka huu akitokea nchini Uganda kupitia mpaka wa Malaba.
Siku ya hapo jana Jumanne mshukiwa anadaiwa kuwasili jimboni Marsabit akiwa na nia ya kuelekea katika taifa jirani la Ethiopia.
Kwa sasa mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Marsabit akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya hapo kesho Alhamisi.
Gachago amepongeza wananchi kwa kutoa taarifa hizo muhimu huku akiomba ushirikiano zaidi katika vita dhidi ya uhalifu.
Aidha ametoa onyo kali kwa walanguzi wa dawa za kulevya akisema kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.



Post Comment