Highlights

Maoni mseto Marsabit kufuatia uwekaji wa kamera za NTSA Barabarani.

Na Nyabande Orwa

Siku chache baada ya mamlaka ya usafiri na usalama barabarani nchini, (NTSA), kuanzisha mchakato wa kukabiliana na ajali za barabarani kwa kuweka kamera za siri katika baadhi ya barabara na kuanza kutoza faini madereva wanaokiuka sheria za trafiki, wakazi, madereva wa matatu pamoja na washikadau wengine wametoa maoni tofauti kuhusu hatua hiyo.

Baadhi ya madereva wa matatu wanaohudumu katika barabara kuu ya Isiolo – Marsabit wanasema hatua hiyo itasaidia kupunguza mienendo mibaya ya baadhi ya madereva wanaokiuka sheria za trafiki kimakusudi ili kupata safari nyingi zaidi na hivyo kuhatarisha maisha ya abiria.

Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa magari ya uchukuzi wanasema sheria hiyo inaweza kuwaathiri zaidi wamiliki wa magari badala ya madereva wanaofanya makosa.

Wakati huo huo, baadhi ya madereva wamepinga uwekaji wa kamera hizo wakisema hautasaidia kupunguza ajali barabarani, badala yake wameitaka pia mamlaka ya NTSA kuimarisha ukaguzi wa vifaa vya kudhibiti mwendo wa magari ya uchukuzi ili kuhakikisha vinafanya kazi ipasavyo.

Aidha, baadhi yao wanasema hatua hiyo huenda isimalize kabisa tatizo la hongo barabarani, wakidai kuwa baadhi ya maafisa wa usalama bado huomba hongo hata magari yanapokuwa katika hali nzuri.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wamekaribisha hatua ya NTSA wakisema kuwa itaongeza usalama barabarani na kuwafanya madereva kuendesha kwa nidhamu zaidi.

Post Comment