Highlights

Marsabit yaadhimisha siku ya wanyama duniani

Na Nyabande Orwa

Kaunti ya Marsabit imeungana na dunia nzima kusherehekea siku ya wanyama duniani mwaka huu chini ya kauli mbiumimea ya dawa na manukato kulinda afya, mila na maisha ya watu.

Akizungumza alipoongoza sherehe hizo katika hifadhi ya Wanyama ya losai, kaunti ndogo ya Laisamis, afisa mkuu wa idara ya wanyama pori (KWS) kanda ya Kaskazini Mashariki, Bakari Chongwa, amesema kuwa mimea ya dawa na manukato inapatikana kwa wingi katika kaunti ya Marsabit.

Amesema mimea hiyo hutumika kutibu magonjwa ya binadamu na wanyama, hutumika katika mapishi na kutengeneza manukato majumbani. Aidha, amesema kuwa mimea hiyo inaweza kuwa chanzo cha kipato kwa wananchi iwapo italindwa na kutumika ipasavyo.

Chongwa amesisitiza kuwa uhifadhi wa mazingira ya asili ni muhimu kwa mustakabali wa kizazi cha sasa na kijacho, na utasaidia kulifanya taifa kuwa na afya bora.

Wakati huo huo, Chongwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miche zaidi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema mabadiliko hayo yamechangia kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyama pori. Amewahimiza wananchi kubuni njia salama za kuishi pamoja na wanyama pori huku wakikabiliana na hali ya mabadiliko ya tabia nchi.

Vilevile, ametoa onyo kali kwa wawindaji haramu katika kaunti ya Marsabit akisema kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Chongwa amesema idara yake imeimarisha operesheni za kuwasaka washukiwa, wakiwemo wanaodaiwa kuuza nyama ya wanyama pori katika mabucha. Ameongeza kuwa wanashirikiana na vyombo vingine vya usalama kuhakikisha wahalifu hao wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Laisamis, Kepha Mwaribe, amewataka wananchi kujiepusha na uharibifu wa misitu hasa kupitia uchomaji wa makaa.

Amesema uhifadhi wa mazingira unaweza kusaidia nchi kunufaika na fedha za wafadhili kutoka mataifa na mashirika mbalimbali, ambazo husaidia katika sekta kama elimu kupitia ufadhili wa masomo unaotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Post Comment