Marsabit kuipa kipaumbele uchimbaji visima na mabwawa kukabili uhaba wa maji.
Na Samuel Kosgei
Idara ya Maji katika Kaunti ya Marsabit imesema kuwa itaipa kipaumbele miradi ya uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa katika bajeti yake ijayo.
Waziri wa Maji na Mali Asili, Guyo Guracha, ameiambia meza ya shajara kuwa wizara yake imeweka uzito katika miradi hiyo ili kupunguza tatizo la maji, hasa wakati wa msimu wa kiangazi.
Aidha, amesema kuwa serikali ya kaunti inaendelea kushirikiana na wafadhili mbalimbali, ikiwemo kupitia Mpango wa Kufadhili Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Zinazoongozwa na Jamii (FLLoCA), kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa maji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Guracha pia amewahimiza wakaazi wa Marsabit kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua inayoendelea kunyesha, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza uhaba wa maji kwa muda mfupi.
Vilevile, amewataka wakaazi kupanda miche ya miti ili kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.



Post Comment