Juhudi zaongezwa kukomesha dhuluma za kijinsia na kulinda haki za msichana.
Na Samuel Kosgei
Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa ukanda wa Mashariki ya Juu imesema inaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali nchini ili kukabili ongezeko la visa vya dhuluma za kijinsia katika eneo hili.
Afisa wa tume hiyo katika ukanda huu Ali Haro Somo, amesema wamebuni mikakati na sera maalum za kukabili unyanyasaji wa kijinsia, akibainisha kuwa hatua hizo zinalenga kupunguza na hatimaye kukomesha vitendo hivyo.
Aidha, amesema kuwa serikali imeanzisha dawati maalum za jinsia katika vituo vya polisi kote nchini ili kurahisisha kuripoti visa vya dhuluma za kijinsia, kurekodi taarifa na kusaidia kufanikisha hatua za kisheria dhidi ya washukiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Jinsia na Utamaduni katika Kaunti ya Marsabit, Armara Galwab, amesema idara ya jinsia ya kaunti imeimarisha mawasiliano kati ya jamii na idara hiyo panapotokea visa vya dhuluma, hasa vinavyowahusu watoto.
Amesema kupitia ushirikiano na mashirika yanayotetea haki za kijinsia kama vile Access to Medicines Platform, wameweza kusaidia waathiriwa kupata haki na huduma muhimu.
Naye afisa kutoka shirika la Access to Medicines Platform, Robert Athewa, amesema katika nyakati za sasa ni muhimu wasichana, hasa kutoka maeneo kame, kuwezeshwa kupata elimu ili waweze kushiriki katika maamuzi muhimu ya jamii na hata ya taifa.
Kauli hizo zinajiri siku moja baada ya ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake iliyoadhimishwa Jumapili. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Haki. Uadilifu. Hatua za Kuchukua kwa Wanawake na Wasichana Wote.”



Post Comment