Wazee wa amani Marsabit wataka serikali kusuluhisha mzozo wa mpaka wa Wajir na Moyale kwa haraka.
Na Samuel Kosgei
Kamati ya Wazee wa Amani kaunti ya Marsabit imeitaka serikali ya kitaifa kusuluhisha haraka mzozo wa mpaka kati ya wakaazi wa Moyale, Marsabit na Eldas, Wajir.
Wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wazee wa Amani, Adan Chukulisa, wazee hao wamesema suala hilo linafaa kupewa uzito unaostahili kwani lisipotatuliwa kwa haraka linaweza kusababisha mivutano na uhasama kati ya jamii hizo mbili jirani.
Chukulisa amesema kabla ya mradi wowote kuanzishwa katika eneo hilo la mpakani, ni muhimu kuwahusisha wakaazi wa eneo linalozozaniwa kwa mujibu wa matakwa ya Katiba.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Amani, Sora Guyo, ametoa wito kwa jamii za Marsabit kuacha tabia ya kuwaficha wahalifu kutoka katika jamii zao, akisema hali hiyo ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuendelea kwa wizi wa mifugo na mashambulizi ya mara kwa mara katika kaunti hii.
Amesema kuwa kuficha wahalifu ni sawa na kushiriki uhalifu kwani kunazuia sheria kuchukua mkondo wake.



Post Comment