Highlights

Wauguzi Marsabit waadhimisha Wiki ya Wauguzi Duniani

Na Joy Akinyi & JB Nateleng

Wauguzi katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Marsabit wameungana na wenzao duniani kuadhimisha wiki ya wauguzi duniani, iliyofikia kilele chake leo tarehe 12 Mei 2026.

Maadhimisho hayo yalianza tarehe 6 Mei kwa lengo la kutambua mchango wa wauguzi katika sekta ya afya pamoja na kuwapa mafunzo ya kuwasaidia kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza na idhaa hii wakati wa maadhimisho hayo, Naibu Mkurugenzi wa wauguzi katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Marsabit, Sadhia Galgallo Odha, amesema wauguzi wana jukumu muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.

Ameongeza kuwa wiki hiyo pia inalenga kuthamini kazi ya wauguzi ambao wameendelea kujitolea kuhudumia jamii licha ya changamoto mbalimbali.

Sadhia ametaja ukubwa wa kaunti ya Marsabit pamoja na upungufu wa wauguzi kuwa baadhi ya changamoto zinazowakabili wanapotekeleza majukumu yao.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mkrugenzi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Marsabit, Kusu Abduba, ambaye amesema hospitali hiyo inahitaji takriban wauguzi 300 lakini kwa sasa ina wauguzi 114 pekee.

Hata hivyo, amesema wauguzi wataendelea kutoa huduma kwa wananchi huku wakitumai idadi ya wahudumu wa afya itaongezeka ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Marsabit na maeneo ya karibu.

Post Comment