Highlights

Marsabit kutawaliwa na ukavu huku mvua  zikitarajiwa kunyesha maeneo ya mpakani – Idara ya hali ya hewa MBT.

Na Samuel Kosgei

IDARA ya Hali ya Hewa Kaunti ya Marsabit imetoa utabiri wa hali ya hewa kwenye ripoti yake ya kila wiki inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya kaunti inatarajiwa kuwa kavu huku mvua zikitarajiwa kunyesha katika maeneo machache ya mpakani mwa Ethiopia.

Kulingana na utabiri huo, wa kuanzia leo tarehe 12th – 18th maeneo ya Dukana, Sololo, Moyale pamoja na maeneo ya karibu na Mlima Marsabit yanatarajiwa kupokea mvua za kiwango cha kati hadi kikubwa katika baadhi ya sehemu, huku maeneo mengi ya ndani yakitarajiwa kupata chini ya milimita moja ya mvua.

Katika eneo la Marsabit Central ikiwemo Marsabit mjini, Sagante/Jaldesa na Karare, mvua nyepesi zinatarajiwa karibu na Mlima Marsabit hasa nyakati za alasiri na jioni, huku maeneo mengi yakisalia na hali ya jua na ukavu kwa muda mwingi wa wiki.

Maeneo ya North Horr na Dukana yanatarajiwa kupokea kiwango kikubwa zaidi cha mvua hasa maeneo ya mpakani mwa Ethiopia ambapo baadhi ya sehemu zinaweza kupata kati ya milimita 10 hadi 40 za mvua.

Katika maeneo ya Laisamis, Logologo, Korr na Ngurunit, hali ya ukavu inatarajiwa kutawala kwa sehemu kubwa ya wiki huku mvua ikiwa kidogo  sana.

Kaunti ndogo ya Moyale ikiwemo Sololo, Uran, Obbu na Butiye inatarajiwa kuendelea kupokea mvua za hapa na pale, ingawa kiwango chake kinatarajiwa kuwa kidogo ikilinganishwa na wiki zilizopita. Maeneo ya mpakani yanaweza kushuhudia radi na mvua za wastani.

Turbi na maeneo yanayozunguka yanatarajiwa kuwa na hali ya joto na ukavu huku mvua zikiwa chache sana.

Katika ukanda wa Loiyangalani na Ziwa Turkana, hali ya joto kali na upepo mkali inatarajiwa kutawala. Upepo huo unaweza kusababisha mawimbi makubwa ziwani, vumbi na kupungua kwa uwezo wa kuona.

Maeneo ya Kargi na South Horr pia yanatarajiwa kubaki makavu kwa sehemu kubwa ya kipindi hicho huku mawingu na manyunyu mafupi yakitarajiwa katika baadhi ya maeneo.

Aidha, idara hiyo imesema maeneo mengi ya kaunti yatashuhudia upepo wa wastani hadi mkali, hasa katika maeneo ya wazi na ya jangwani.

Post Comment