Watu watatu wapigwa risasi mguu wa kushoto kila mmoja katika jaribio la wizi, Merille
Na Caroline Waforo.
Maafisa wa polisi katika kaunti ya Marsabit wanachunguza tukio na ambapo watu watatu walijeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la kibiashara la Merille kaunti ndogo ya Marsabit South usiku wa jana Jumanne.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi kaunti ya Marsabit Leonard Kimaiyo amesema kuwa wanandoa pamoja na mfanyikazi wao mmoja walikuwa wakielekea nyumbani baada ya kufunga kazi majira ya saa nne usiku walipovamiwa na watu watatu waliokuwa wamejihami, katika tukio linaloshukiwa kuwa jaribio la wizi.
Kamanda Kimaiyo amesema watatu hao walipigwa risasi mguu wa kushoto kila mmoja huku akidokeza kuwa hakuna fedha wala mali iliyoibwa, baada ya waathiriwa hao kufanikiwa kutupa pesa walizokuwa nazo katika boma la jirani.
Majeruhi wanapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Meru huku maafisa wa polisi wakiendelea na msako wa kuwatafuta washukiwa wa tukio hilo.



Post Comment