Highlights

Jamii yalaumiwa kwa kutelekeza jukumu la kulinda haki za watoto wa kike, Marsabit

Na JB Nateleng

Jamii katika kaunti ya Marsabit imelaumiwa kwa kushindwa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya dhulma za kijinsia ikiwemo mimba za mapema, huku wanaowahusisha na vitendo hivyo wakiachwa huru bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kauli hiyo imetolewa na msimamizi wa shirika la World Vision kaunti ya Marsabit, James Jarso, ambaye amesema wazazi wengi wamepuuza wajibu wao wa kulinda haki za watoto kwa kuripoti visa vya dhulma dhidi ya watoto wao kwa vyombo vya usalama.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Elimu ya Jimbo Katoliki la Marsabit, ambapo pia Shule ya Msingi ya Loiyangalani ilikuwa ikiadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, Jarso amesema jamii inaendelea kupoteza mwelekeo huku watoto wa kike wakibebeshwa majukumu ya uzazi katika umri mdogo.

Jarso pia aliwatuhumu baadhi ya walimu na wadau wa elimu kwa kushindwa kusimama kidete kulinda watoto dhidi ya dhulma, huku akisema baadhi yao wamekuwa sehemu ya tatizo linalowakumba wanafunzi wa kike.

Aidha, amekosoa idara za usalama kwa kile alichotaja kuwa uzembe katika kushughulikia kesi za watoto waliodhulumiwa, akitaka viongozi wa usalama katika kaunti ya Marsabit kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua na waathiriwa wanapata haki.

Kadhalika, Jarso ametoa wito kwa viongozi wa dini, serikali pamoja na wadau wengine kushirikiana katika kubuni mazingira salama yatakayowalinda watoto dhidi ya dhulma za kijinsia na mila potovu zinazoathiri elimu ya mtoto wa kike.jar

Post Comment