Highlights

Wanaharakati wataka polisi wachukuliwe hatua kwa kudaiwa kumshambulia kijana mmoja mjini Marsabit

Na Samuel Kosgei

Wanaharakati wa haki za binadamu kaunti ya Marsabit wanazitaka idara za usalama kuwachukulia hatua kali maafisa wa polisi wanaodaiwa kumuumiza kijana mmoja wakati wa maandamano ya kupinga mzozo wa mpaka kati ya Marsabit na Wajir Alhamisi iliyopita.

Wakiongozwa na mwanaharakati Hassan Mohammed, wanaharakati hao wamedai kuwa kijana huyo alipigwa vibaya na maafisa wa polisi na kusababisha kuvunjika kwa kidole pamoja na kuumia mkono.

Akizungumza na wanahabari mjini Marsabit, Mohammed amesema kuwa mwathiriwa kwa jina Mohamud Yusuf hakuwa akishiriki maandamano wala kufanya kosa lolote, bali alikuwa akiendelea na shughuli zake katika afisi za basi la Mabruk mjini Marsabit aliposhambuliwa na askari hao, hali iliyomsababishia majeraha makubwa.

Mohammed sasa anaitaka Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi nchini IPOA kuchunguza kwa kina tukio hilo la dhulma za polisi ili maafisa waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria. Pia amesisitiza kuwa mwathiriwa anapaswa kupata haki.

Wakati huo huo, mwanaharakati huyo amewataka waandamanaji wanaojihusisha na uharibifu wa mali na wizi wakati wa maandamano kuacha tabia hiyo, akisema kuwa vitendo hivyo haviwezi kuwa sehemu ya kudai haki.

Aidha, ameonyesha masikitiko yake kufuatia baadhi ya vijana kuchoma barabara ya lami wakati wa maandamano, akisema kuwa hiyo ndiyo njia kuu inayounganisha kaunti ya Isiolo na Marsabit, hivyo haifai kuharibiwa.

Post Comment