Vijana mjini Marsabit washiriki maandamano kulalamikia unyakuzi wa ardhi inayozozaniwa mpakani mwa Marsabit na Wajir.
Na JB Nateleng
Vijana mjini Marsabit wameshiriki maandamano leo alhamisi kulalamikia kile wanadai ni unyakuzi wa ardhi inayozozaniwa ya Basir mpakani mwa Marsabit na Wajir.
Waandamanaji hao pia wametaka kuachiliwa huru kwa kwa aliyekuwa chifu wa Golole, Dabassa Dambi, pamoja na Mzee Guracha Dambala waliokamatwa siku ya Jumamosi wakihusishwa na Kundi la Oromo Liberation Army.
Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa vijana katika kaunti ndogo ya Saku, Guyo Kacharo, amesema kuwa serikali ina jukumu la kuhakikisha usalama na haki za wananchi wote akiitoa wito kwa idara za usalama kuharakisha uchunguzi wa suala hilo na kutoa taarifa rasmi kuhusu hatua zilizochukuliwa.
Kacharo pia amehimiza kuimarishwa kwa usalama katika maeneo ya mpakani kati ya Marsabit na Wajir, akisema hatua hiyo itasaidia kulinda maisha na mali ya wananchi.
Aidha, amependekeza kuwepo kwa mazungumzo ya pamoja kati ya jamii husika na mamlaka ili kupata suluhu ya kudumu kuhusu masuala yanayoibuliwa na wakazi.
Kauli yake imeungwa mkono na baadhi ya vijana kutoka eneo la Saku wanaoitaka serikali kushughulikia suala hilo kwa njia ya haki na uwazi.
Wametoa wito kwa viongozi wa usalama katika kaunti hiyo, wakiongozwa na Kamishna wa Kaunti James Kamau, kusaidia kudumisha utulivu na kuimarisha maelewano miongoni mwa jamii.
Vijana hao pia wametoa wito kwa Rais William Ruto kuhakikisha kuwa haki inazingatiwa kwa wote wanaohusika, huku wakisisitiza umuhimu wa amani, mshikamano na kufuatwa kwa sheria katika kushughulikia masuala ya usalama.



Post Comment