Wakaazi Marsabit wahimizwa kutunza misitu
Na JB Nateleng
Wito wa kutunza misitu na mazingira umetawala kwenye maadhimisho ya Siku ya Bioanuwai Duniani, yaliyofanyika leo Ijumaa katika eneo la Karare kaunti ya Marsabit.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mkuu wa Idara ya wanyama pori (KWS) kanda ya Kaskazini Mashariki, Bakari Chongwa, amesema kuwa utunzaji wa misitu una manufaa makubwa kwa jamii na mazingira.
Chongwa amesema KWS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika shughuli za upandaji miti pamoja na kubuni mbinu mbadala za kuhifadhi misitu ili kusaidia kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na wananchi wanaoishi karibu na mbuga za wanyama.
Aidha, amesema serikali inaendelea kuimarisha sekta ya utalii Marsabit kwa lengo la kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea mbuga za wanyama pamoja na mandhari ya kipekee yanayopatikana katika kaunti ya Marsabit
Wakati uo huo Naibu Kamishna wa Marsabit Central, Mathew Wambugu amewahimiza wazee wa jamii za Marsabit kuchukua jukumu la kuwafunza vijana umuhimu wa kuhifadhi na kutunza miti asilia kwa manufaa ya jamii na mazingira.



Post Comment