Highlights

Serikali yatoa shilingi milioni 24.3 kufidia waathiriwa wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori Marsabit

Na JB Nateleng

Serikali kupitia Idara ya Huduma za Wanyamapori nchini, (KWS), imetoa jumla ya shilingi milioni 24.3 kufidia waathiriwa 155 wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika kaunti ya Marsabit.

Walionufaika ni wakazi walioathirika na mgogoro wa wanyamapori kati ya mwaka 2014 hadi 2021.

Kupitia hotuba ya waziri wa utalii na wanyamapori Rebecca Miano iliyosomwa na Tobiko Nayioma, ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala katika wizara hiyo, amesema kuwa serekali imejitolea kuhakikisha malalamishi ya waathiriwa yanashughulikiwa kwa wakati unaofaa.

Miano amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu kwa kuongeza idadi ya maafisa wa KWS na kujenga uzio wa kuzuia wanyamapori kuvamia makazi ya wananchi hatua inayolenga kupunguza visa vya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.

Aidha, Miano amesema ushirikiano kati ya serikali kuu na kaunti ya Marsabit umechangia kukuza utalii nchini, huku akiahidi kuwa wakazi wa eneo hilo watanufaika zaidi kupitia sekta hiyo.

706028794_1461506389324443_9029037067398221707_n-1024x771 Serikali yatoa shilingi milioni 24.3 kufidia waathiriwa wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori Marsabit
Afisa mkuu katika idara ya Maliasili na wanyamapori Marsabit Pauline Marleni akimkabithi muathiriwa fidia kutoka KWS

Wakati huo huo, afisa mkuu katika idara ya maliasili na wanyama pori, kaunti ya Marsabit Pauline Marleni ameihimiza Idara ya utalii na wanyamapori kuongeza hamasa kwa wananchi kuhusu njia sahihi za kuripoti visa vya mashambulizi ya wanyamapori.

Amesema wengi wa waathiriwa bado hawajaripoti matukio hayo kutokana na ukosefu wa ufahamu wa utaratibu unaofaa.

Marleni ameongeza kuwa fidia hiyo imetolewa wakati ambapo mamlaka ya kitaifa ya usimamizi wa mazingira NEMA, kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Marsabit, inajiandaa kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani tarehe 5 Juni mwaka huu.

Hafla ya kuwafidia waathiriwa hao iliandaliwa leo Ijumaa katika shule ya upili ya Karare.

Post Comment